Kufuatia majibu ya kulipiza kisasi ya China na Umoja wa Ulaya kwa sera za Trump za ushuru, Rais wa Marekani ameongeza ushuru kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka China hadi 104%. Kwa hatua hii ya Trump, soko la hisa la Marekani liliendelea kuporomoka kwa siku ya nne mfululizo Jumanne wiki hii.
Marekani ilitangaza ushuru mwingine wa asilimia 50 kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka China baada ya Beijing kukataa kulegeza kamba katika msimamo wake wa kutoza ushuru ziada wa asilimia 34 kwa bidhaa za Marekani ili kulipiza kisasi cha nyongeza ya ushuru iliwekwa na Trump, kufikia mchana Jumanne. Trump aliandika kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii, Truth Social kwamba: "Licha ya onyo langu kwamba nchi yoyote ambayo italipiza kisasi dhidi ya Merekani kwa ushuru itakabiliwa mara moja na ushuru wa juu zaidi, China imejibu kwa kuweka ushuru mpya na wa juu zaidi wa kulipiza kisasi wa 34% ..."
Msemaji wa Wizara ya Biashara ya China amesema: "Tishio la Marekani la kuongeza ushuru zaidi ni kosa juu ya makosa mengine, na kwa mara nyingine linaweka wazi dhati ya dhulma na uonevu ya Marekani... China haitakubali kamwe jambo hili." Mojawapo ya matokeo ya sera za utozaji ushuru mkubwa za Trump ni kukaribiana zaidi mihimili ya kiuchumi ili kupunguza athari mbaya za sera za ushuru za Marekani. Umoja wa Ulaya ni mshirika wa Marekani, na China inatambuliwa na Marekani kama mshindani na adui katika uga wa kimataifa. Sasa, Umoja wa Ulaya unafanya uratibu zaidi na China kuhusu sera za biashara ili kukabiliana na sera za ushuru za Trump.
Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen amezungumza kwa njia ya simu na Waziri Mkuu wa China, Li Keqiang kuhusu hali ya uhusiano wa pande hizo mbili na masuala ya kimataifa. Mazungumzo hayo yamefanyika kwa mnasaba wa maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya pande hizo mbili. Von der Leyen alisisitiza udharura wa kukabiliana na adui wa pamoja, yaani Marekani akisema kwamba: "Ulaya na Uchina, kama masoko mawili makubwa ya kimataifa, zina jukumu la pamoja la kulinda mfumo wa biashara uliorekebishwa, huru, wa haki na wenye ushindani."
Mojawapo ya nyakati muhimu za uratibu katika vita vya biashara duniani utakuwa mwezi Julai; Wakati Umoja wa Ulaya unatarajia kuwakaribisha maafisa wa ngazi za juu wa China. Ripoti zinasema, mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya na China umepangwa kufanyika mjini Brussels mwezi Julai. Maafisa wa Ulaya wanauona mkutano huo kuwa ni fursa ya kutafakari upya uhusiano wa kibiashara na kistratijia wa pande hizo mbili katika zama za baada ya Trump na kuimarisha kujitawala kimkakati Ulaya dhidi ya mashinikizo ya kiuchumi ya nje. Ushuru wa kibiashara wa zaidi 100% wa Marekani kwa bidhaa za China pia umezitia nchi za Ulaya wasiwasi wa kuongezeko mauzo ya bidhaa za China kwenda Ulaya.
Kwa mujibu wa Financial Times, ukali wa ushuru wa Trump kwa chumi kama za China na Vietnam una maana kuwa Brussels sasa inajiandaa kwa utitiri wa bidhaa za Asia kama vile bidhaa za umeme na mashine. Maafisa wa Ulaya wanasema Tume ya Ulaya inatayarisha ushuru mpya wa dharura ili kukabiliana na ushuru wa Marekani na wamezidisha ufuatiliaji wa mtiririko wa bidhaa katika masoko ya bara hilo. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana wataalamu wanasema kuwa, sera za ushuru za Trump zimevuruga utaratibu wa biashara ya kimataifa na mikataba ya Shirika la Biashara Duniani.
Weledi wengi wa masuala ya kiuchumi wanaamini kuwa vita vya kibiashara vilivyoanzishwa na Trump havina mshindi na kwamba mataifa yote makubwa kiuchumi duniani, ikiwemo Marekani, yatapata hasara.
342/
Your Comment